Türk  ataka uwajibikaji wa vikosi vya usalama Nepal na waandamanaji wazingatie kanuni
10 September 2025

Türk ataka uwajibikaji wa vikosi vya usalama Nepal na waandamanaji wazingatie kanuni

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu ameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia ghasia zinazoendelea na kushika kasi nchini Nepal, huko barani Asia, ambako maandamano dhidi ya ufisadi na marufuku ya mitandao ya kijamii yamesababisha vifo vya watu wengi pamoja na majeruhi. Flora Nducha amefuatilia taarifa hiyo na anatupasha zaidi.Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, akizungumza mjini Geneva amesema“nimeshtushwa na ongezeko la ghasia nchini Nepal ambalo limesababisha vifo kadhaa na kujeruhi mamia ya waandamanaji wengi wao wakiwa vijana, pamoja na uharibifu mkubwa wa mali.”Katika siku za karibuni, maandamano yaliyoanzia katika mji mkuu Kathmandu sasa yamesambaa katika miji na vijiji vya Nepal, yakiacha barabara zikifunikwa na mabaki ya vitu vilivyoteketezwa kwa moto na kulazimisha maduka kufungwa pia kuhofia usalama.Kwa mujibu wa duru za habari maandamano hayo yanayoo nngozwa na vijana wa kati ya umri wa miaka 13 hadi 28 au Gen Z yameshakatili Maisha ya takribani watu 22, kusababisha waziri mkuu wa nchi hiyo KP Sharma Oli kujiuzulu na kuliwasha moto jengo la bunge .Türk ametoa wito kwa vikosi vya usalama kujiepusha na mapambano na waandamanajI akisema, “Naomba vikosi vya usalama waoneshe uvumilivu wa hali ya juu, na kuepusha umwagaji damu na madhara zaidi. Vurugu siyo suluhisho. Mazungumzo ndiyo njia bora na ya pekee ya kushughulikia malalamiko ya watu wa Nepal. Ni muhimu sauti za vijana zisikike.”Waandamanaji wanasema wameshikwa na hasira kutokana na ufisadi na marufuku ya serikali juu ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, ingawa kwa sasa huduma za mitandao ya kijamii zimerejea. Türk anasema anatambua haki yao ya kusikika, lakini pia amewasihi wawe na uwajibikaji.“Nawakumbusha waandamanaji kuwa nao pia lazima washikamane na kuzingatia dhamira ya kukusanyika kwa amani na wajiepushe na ghasia.”Türk ametaka uchunguzi wa haraka, wa wazi na huru ufanyike kuhusu madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi ya vikosi vya usalama, huku pia akilaani mashambulizi dhidi ya majengo ya umma, biashara, na hata maafisa waandamizi wa serikali.Amesisitiza kuwa dunia inathamini safari ya Nepal kutoka kwenye migogoro hadi kuwa na demokrasia yenye amani na ametoa mwito kwa wadau wote kulinda mafanikio hayo. Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia kupitia mazungumzo na hatua za kujenga imani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza mvutano na kurejesha hali ya utulivu.