17 August 2026
Sudan Kusini : Wakimbizi wako hatarini kukosa chakula yasema UN
Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
About
Zaidi ya wakimbizi na waomba hifadhi 650,000 nchini Sudan Kusini wako katika hatari ya kupoteza msaada muhimu wa chakula na lishe kutokana na ukosefu mkubwa wa fedha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, na lile linalohusika na masuala ya wakimbizi UNHCR zimeonya. Kupunguzwa kwa msaada kunaweza kuwaathiri wakimbizi 240,000 ndani ya wiki chache, wakati nchi hiyo yenyewe ikikabiliwa na ongezeko la tatizo la njaa. Feissal Kirwa na taariifa zaidi(TAARIFA YA FEISSAL KIRWA)Nattss…..Katika makazi ya wakimbizi ya Wedweil nchini Sudan Kusini, akina mama na watoto wanasubiri msaada wa chakula na lishe ambao wengi wanategemea ili kuendelea kuishi.Zaidi ya watu milioni 7.8 nchini Sudan Kusini ambani zaidi ya nusu ya idadi ya watu wote wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku watoto milioni 2.2 wakikabiliwa na unyafuzi.Sasa, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa wakimbizi wanaofika nchini humo wakiwa tayari na utapiamlo mkubwa wanaweza kukabiliwa na hali mbaya zaidi iwapo ufadhili utaisha.Katika vituo vya lishe, watoto hupimwa uzito na urefu huku wahudumu wa afya wakifuatilia hali yao, wakati akina mama wakipewa chakula cha ziada kwa ajili ya watoto wao. Naibu Mkuruengenzi wa WFP nchini Sudan Kusini ni Adham Effendi,(SAUTI YA ADHAM EFFENDI- RASHID)“Bila ufadhili wa haraka, msaada kwa zaidi ya wakimbizi 650,000 utapunguzwa, na hivyo kuweka maisha na mustakabali wao hatarini. Hii inaweza kumaanisha mgao mdogo wa chakula na kupunguzwa kwa msaada wa lishe kwa watoto na akina mama.”Kwa wakimbizi wengi wapya, msaada huanza mara tu wanapowasili Sudan Kusini. Biskuti zenye virutubisho na za kutia nguvu hutolewa kwa watu ambao huenda hawana sehemu za kupikia au maji safi.Lakini wimbi la watu wanaokimbia migogoro linaendelea kuongezeka.Idadi ya wakimbizi na watu wanaorejea nchini humo takrivab 3,000 wanafika Sudan Kusini kutoka Sudan kila wiki, na kuongeza shinikizo kwa jamii na huduma ambazo tayari zimeelemewa. Adham anaongeza(SAUTI YA ADHAM EFFENDI 2- RASHID)“Msaada wa chakula mara nyingi ndio tofauti kati ya kukabiliana na hali ngumu na janga. Pamoja na washirika wetu UNHCR na wengine, WFP inawasaidia wakimbizi na jamii zinazowapokea. Lakini mahitaji yanaongezeka kwa kasi zaidi kuliko rasilimali zilizopo.”Baadhi ya familia sasa zimejikuta zikilala chini ya miti baada ya kukimbia Sudan.Miongoni mwao ni Saleh, anayepika chakula cha mchana huku mke wake akimtunza mtoto wao wa miezi sita.Wengine, kama Esraa, wameishi katika makazi hayo ya wakimbizi kwa miaka kadhaa. Msaada wa fedha kutoka WFP umemsaidia kununulia familia yake chakula na kuendesha biashara yake ndogo.Lakini msaada huo muhimu sasa uko hatarini kutoweka.WFP na UNHCR zinasema uhaba wa fedha unaweza kulazimisha kupunguzwa kwa mipango ya chakula na lishe kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi na waomba hifadhi.Mashirika hayo yanaonya kuwa kupungua kwa msaada kunaweza kusababisha ongezeko la utapiamlo miongoni mwa watoto, huku wanawake na watoto wakikabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kukatili na kudhulumiwa.Huku njaa ikiwa tayari imeenea nchini Sudan Kusini na wakimbizi wapya wakiwasili kila wiki, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanatoa wito wa ufadhili wa haraka ili kuzuia hali kuzorota zaidi na kulinda familia zilizo katika mazingira hatarishi dhidi ya njaa kali na utapiamlo.