Skip to content
Opens in a new window
Licha ya changamoto mijini, Somalia yafanikisha kampeni ya chanjo ya polio
17 August 2026

Licha ya changamoto mijini, Somalia yafanikisha kampeni ya chanjo ya polio

Habari za UN - Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

About
Zoezi la siku tano la utoaji chanjo dhidi ya polio limekamilika katika mkoa wa Banadir nchini Somalia, likiwafikia watoto zaidi ya 122,000 walio chini ya umri wa miaka mitano. Kampeni hiyo imeendeshwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Somalia, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wengine. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Flora Nducha.(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)Kampeni hiyo imetekelezwa katika wilaya za Daynile, Garasbaley na Kahda, ambako kuna familia nyingi zilizolazimika kuyakimbia makazi yao na ambazo imekuwa vigumu kuwafikia watoto wao katika kampeni zilizopita.Kwa muda wa miezi mitatu, Wizara ya Afya ya Somalia, utawala wa mkoa wa Banadir, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF na wadau wengine walifanya maandalizi ya kina ili kuwafikia watoto walio hatarini zaidi.Katika utekelezaji wake, timu 178 zilitumwa kutoa chanjo ya matone dhidi ya polio nyumba kwa nyumba, katika vituo maalumu, maeneo ya vituo vya mpito na kupitia timu zinazohamahama.Timu hizo zilitumia takwimu za idadi ya watu, ramani za kijiografia na taarifa kutoka maeneo husika kutambua makazi na watoto ambao hawajapata chanjo.CHANGAMOTO MIJINIKatika taarifa yake kutoka Mogadishu nchini Somalia, WHO imeeleza  kuwa kufikia kila mtoto katika maeneo ya mijini bado ni changamoto.Mkoa wa Banadir unapokea watu wengi wanaokimbia maeneo mengine kutokana na ukosefu wa usalama nchini Somalia. Baadhi yao huishi katika makazi yasiyo rasmi na kuhama mara kwa mara, hali inayofanya iwe vigumu kuwatambua na kuwafuatilia watoto ambao hawajapatiwa chanjo.Licha ya changamoto hizo, watoto 122,067 walipatiwa chanjo, sawa na asilimia 94 ya lengo la awali. Juhudi zinaendelea, watoto waliokosa chanjo watatafutwa na kupatiwa huduma hiyo haraka.Mwakilishi wa WHO nchini Somalia, Dkt. Mohamed Ali Kamil, amesema “Kumfikia kila mtoto kunahitaji uongozi imara wa serikali, ushiriki wa jamii na ushirikiano madhubuti wa wadau wote. Kampeni hii ni fursa muhimu ya kujaribu mbinu inayolenga zaidi mahitaji na kuimarisha uwajibikaji katika utoaji chanjo mijini.”KWA NINI CHANJO YA POLIO?Chanjo hiyo ni muhimu kwa sababu polio inaweza kusababisha ulemavu wa kudumu, lakini pia inaweza kuzuilika kwa chanjo.Somalia imekuwa ikikabiliana na mlipuko wa polio tangu mwaka 2017, hivyo kumfikia kila mtoto ni hatua muhimu katika kuziba pengo la kinga, kukomesha maambukizi na kulinda kizazi kijacho.