About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo juzi Jumanne na jana Jumatano wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa walipata fursa kunadi serra zao mbele ya nchi wanachama kwenye Baraza Kuu wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia walioweza kuwauliza maswali. Miongoni mwa wawakilishi hao ni Irene Kitoti, Mwanzilishi na mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Genesis For Children Organization ya nchini Tanzania aliyezungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili. Pia tunakuletea muhtasari wa habari kama zifuatazo.Kutokana na mafanikio ya kihistoria kwa afya ya umma ya eneo la Karibe, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO limeipongeza nchi ya Bahamas kwa kuwa taifa la hivi karibuni zaidi katika ukanda huo wa Karibe kuthibitishwa kuwa limekomesha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus, kupitia taarifa ya shirika hilo ameipongeza Bahamas kwa mafanikio haya makubwa, yanayoimarisha miaka ya dhamira ya kisiasa na kujitolea kwa wahudumu wa afya.Ikiwa leo imetimia miaka 15 tangu kuanza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasilino, TEHAMA au ICT, Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU), Doreen Bogdan-Martin katika ujumbe wake mahususi wa maadhimisho ya mwaka huu amesema, “kwa sasa tunaishi katika kipindi cha mabadiliko makubwa na ya kusisimua zaidi ya kiteknolojia katika historia ya binadamu lakini vilevile kwa sasa fursa zinazohusiana na mabadiliko haya ya kiteknolojia hazimfikii kila mtu kwa usawa”.Mgogoro wa usafirishaji katika Mlango Bahari wa Hormuz uliosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati umefichua tishio jipya: upungufu  wa madini ya kimkakati yanayoendesha uchumi duniani kote  na sasa nchi huenda zitaanza kuhaha kuyapata. Katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Geneva Uswisi, Dario Liguti, Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Endelevu cha Tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ulaya, UNICE amesema,  “hatua ya kwanza, mbali na ongezeko la bei bila shaka, itakuwa viwanda kupunguza matumizi yake yake ya madini ya kimkakati na hivyo kupunguza uzalishaji… iwe ni paneli za sola, sumaku, betri na kadhalika, katika siku zijazo.”Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "KUPARAMA"Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!