About
Hii leo jaridani tunaangazia sitisho la mapigano katika Mashariki ya kati, kilimo endelevu kinachowakwamua wakimbizi na wenyeji Kakuma nchini Kenya, na mafunzo ya UNDP ya uchimbaji salama wa madini ya ujenzi nchini Tanzania.Umoja wa Mataifa umekaribisha tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuongeza muda wa sitisho la mapigano kati ya Marekani na Iran, ukisema hiyo ni hatua muhimu kuelekea kupunguza mvutano kati ya mataifa hayo mawili.Maisha ya wakimbizi katika eneo la Kakuma, kaskazini mwa Kenya, yanaanza kubadilika kwa kasi kupitia miradi ya kilimo na lishe inayowezeshwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Mpango wa Chakula Duniani  (WFP) na la Chakula na Kilimo (FAO). Kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Turkana chini ya ufadhili wa  Muungano wa Ulaya (EU) sasa wakimbizi wana uwezo wa kuzalisha chakula chao wenyewe, kuboresha lishe, na kujenga maisha ya kujitegemea.Shirika la Umoja wa Mataifa  la Mpango wa Maendeleo (UNDP), kwa kushirikiana na Tume ya Madini nchini  Tanzania katikati mwa wiki iliyopita yaani Aprili 16 na 17 wamefanya warsha ya mafunzo mkoani Singida katikati mwa nchi. Mafunzo hayo yamelenga kuimarisha ujuzi wa uchimbaji salama, unaozingatia sheria, na wenye faida kwa wanawake na vijana wanaojihusisha na uchimbaji mdogo wa madini ya ujenzi.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!