
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina tukimsikia Barbara Batte Guevara, Mkufunzi anayefundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba. Kwa kushirikiana na Tanzania chuo hicho ambacho mwezi uliopita kimetimiza miaka 298 tangu kuanzishwa kwake, hivi karibuni kimetoa fursa kwa Wacuba kujifunza lugha ya Kiswahili.Anold Kayanda wa Idhaa hii amemtembelea Profesa Barbara Batte katika jiji la Havana nchini Cuba ili kufahamu zaidi kuhusu hatua hii na mafanikio yaliyofikiwa hadi kufikia sasa. Pia tunakuletea habari kwa ufupi kama zifuatazo.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa Akili Mnemba au AI wenye thamani ya dola bilioni 3, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inawanufaisha watu wote duniani, badala ya kuwa mali ya mataifa machache au kampuni chache zenye nguvu. Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili Athari za AI huko New Delhi nchini India, Guterres amesema mustakabali wa AI unapaswa kujengwa kwa ushirikiano wa kimataifa”.Mashambulizi makali yanayoendelea kufanywa na Israeli dhidi ya maeneo ya Palestina ya Gaza na Ukingo wa Magharibi ambayo inakalia kimabavu yanatia hofu ya uwezekano wa utokomezaji wa kabila, imesema Ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR), ya kuanzia Novemba 1 2024 hadi Desemba 31 2025. Ripoti inasema mashambulizi ya Israeli yameweka mazingira ambamo kwamo wapalestina kama kundi watashindwa kuendelea kuishi Gaza huku Ajith Sunghay, Mkuu wa Ofisi ya OHCHR Palestina akisema, “ripoti inachambua mwenendo wa mapigano ya jeshi la Israeli, linaloendelea kuua idadi kubwa ya raia, kusababisha njaa, kuwahamisha takribani wakazi wote wa Gaza, tena zaidi ya mara moja — na kuharibu miundombinu iliyosalia ya kiraia ya Gaza.”wanamgambo wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan walitekeleza kampeni iliyoratibiwa ya uharibifu dhidi ya jamii zisizo za kiarabu ndani ya mji wa El-Fasher na viunga vyake, kampeni yenye viashiria vya mauaji ya kimbari, imeeleza ripoti mpya iliyotolewa leo na Tume Huru ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Ukweli kuhusu Sudan. Ripoti imetaja vitendo hivyo ni pamoja na kuua wanachama wa kundi la kikabila linalolindwa; kusababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili; ambavyo ni vipengele muhimu vya kosa la mauaji ya kimbari chini ya sheria za kimataifa.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili tunawasikiliza baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Havana wanaojifunza lughaya Kiswahili. Tuanze na Yibran Nunez Batte.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!