
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoangazia siku ya chakula duniani ikienda sambamba na maadhimisho ya miaka 80 ya kuanzishwa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, na utamsikia Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania Bi. Nyabenyi Tito Tipo akieleza.Maadhimisho ya siku ya chakula duniani yamefanyika kimataifa leo huko Roma nchini Italia, yakienda sambamba na sikukuu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo, FAO. Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema, “Miaka themanini iliyopita, katika dunia iliyosambaratishwa kwa vita, nchi zilikutana kukabiliana na njaa. Miongo kadhaa tangu wakati huo, dunia imepiga hatua kubwa. Lakini bado majanga yanyoonesha kuwa hatuwezi kubweteka iwapo tunataka kuendeleza mafanikio tuliyopata. Tuna mbinu, ufahamu, rasilimali za kutokomeza njaa, na kupatia kila mtu chakula kizuri na chenye afya. Tunachohitaji ni umoja.Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, raia wamerejea kufuatia makubaliano ya sitisho la mapigano lakini wanahaha kujenga upya makazi yao huku wakiwa wamezingirwa na vifusi. Miongoni mwao Ayman Awadallah, amesema “hakuna maji, hakuna miundombinu ya majitaka, hakuna maisha hapa, hakuna chochote.”Na kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kilichotokea Jumatano Oktoba 15 nchini India, Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu umetuma salamu za rambirambi na kusema hayati Odinga, alikuwa mtu muhimu katika maendeleo ya kidemokrasia nchini Kenya na pia mtetezi thabiti wa mageuzi ya kikatiba na utawala jumuishi.Na katika kujifunza Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana za neno "KIMWA"Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!