
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania kwa Chama cha Wanawake Majaji, (TAWJA) ambacho kimetambua pengo la upatikanaji wa haki hususan kwa wanawake na wasichana na tunasikia hatua zinazochukuliwa kuziba pengo hilo kutoka kwa mwenyekiti wake, Barke Sehel ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Pia tunakuletea mhtasari wa habari kama zifuatazo..Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametangazwa kwa mara nyingine kugundulika kwa virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC katika jimbo la Ituri lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hii ni mara ya 17 kwa mlipuko wa Ebola kutokea DRC tangu kugunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976. Wagonjwa 13 vimethibitishwa na taasisi ya utafiti wa tiba ya INRB mjini Kinshasa. Dkt. Tedros amesema tayari wametuma wataalamu, vifaa tiba na ameruhusu kutolewa kwa dola laki tano kusaidia kudhibiti mlipuko huo na kuwahudumia wagonjwa.Hali ya kibinadamu nchini Somalia inazidi kuwa mbaya kuliko ilivyotarajiwa hapo awali. Akuzungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi afisa mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia George Conway amesema “Hivi sasa Takriban watu milioni sita nchini Somalia amba ni sawa na mtu mmoja kati ya sita anakabiliwa na njaa ikimaanisha kuwa anaruka muda wa kula chakula, au anaenda siku kadhaa bila chakula cha kutosha. Watoto ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi. Karibu watoto milioni mbili wana utapiamlo mkali, ikimaanisha kuwa wana utapiamlo mbaya na dhaifu kimwili, na hivyo kuwaweka katika hatari kubwa ya kuugua au kufa.”.Na leo ni siku ya Kimataifa ya Familia, Umoja wa Mataifa unasema maadhimisho ya mwaka huu yanaangazia jinsi umaskini, ukosefu wa huduma muhimu na msaada mdogo wa malezi vinavyoathiri familia na kudhoofisha maendeleo bora ya watoto. Maadhimisho ya mwaka huu yanaweka mkazo maalum kwenye hatua jumuishi za ulinzi wa kijamii kama vile ruzuku za watoto, likizo za uzazi zenye malipo, huduma nafuu za malezi ya watoto na elimu ya awali kwa watoto wadogo.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!