12 NOVEMBA 2025
About
Hii leo jaridani tunaangazia ripoti ya FAO ya uhaba wa chakula, Mwanaharakati kijana kutoka Kenya katika mkutano wa pili wa WSSD Doha, na mradi wa Mifereji ya Maji wa Jiji la Kampala (Kampala Capital City Drainage Master Plan) inayosaidia kupunguza mafuriko Uganda.Ripoti mpya ya pamoja kutoka mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) inaonya kwamba uhaba mkubwa wa chakula unazidi kuongezeka katika maeneo 16 yenye njaa duniani, hali inayoweza kusababisha mamilioni zaidi ya watu kukumbwa na njaa kali au hatari ya kufikia kiwango cha baa la njaa.Mkutano wa Pili wa Dunia wa Maendeleo ya Kijamii umefunga pazia mjini Doha, Qatar, mwishoni mwa wiki hii, ukiwaleta pamoja viongozi wa dunia, mashirika ya kiraia na vijana wakitoka na wito wa pamoja dhidi ya umasikini, ukosefu wa usawa na kutengwa kijamii. Kutoka Kenya, mwanaharakati kijana amesema mkutano huo umekuwa wa kuhamasisha akitoa wito wa hatua za haraka.Kituo cha utafiti wa kusaka Suluhu kuhusu mafuriko kinachoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) nchini Uganda kimetumia maarifa ya pamoja kukabiliana na changamoto za mafuriko katika eneo la Makerere Kavule, makazi yasiyo rasmi yaliyo pembezoni mwa mji wa Kampala, mji mkuu wa Uganda. Kituo hicho kimeunganisha juhudi za jamii, maarifa asilia, na teknolojia ya kisasa kubuni mfumo wa mifereji ya maji unaoendana na Mpango Mkuu wa Mifereji ya Maji wa Jiji la Kampala (Kampala Capital City Drainage Master Plan). Mfumo huu unalenga kupunguza mafuriko si tu katika jamii hiyo, bali pia katika eneo la katikati ya jiji.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!