
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayomulika ujumbe wa Omon Ukpoma-Olaiya, Kiongozi wa Uwekezaji wa UNCDF kwa Kanda ya Afrika Mashariki, Kusini na Nchi za Kiarabu. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na uchambuzi neno la wiki.Haiti, hali ya kibinadamu imefika kiwango cha hatari, amesema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk. Akihutubia Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Türk amesema Haiti imefika kiwango cha kulipuka kutokana na ukatili na ukiukwaji Mkubwa wa haki za binadamu. Amesisitiza kuwa “Tunaweza na lazima kubadili hali hii kwa ajili ya watu wa Haiti,” akiongeza kuwa “bila hatua za haraka hali mbaya zaidi huenda ikaja kwa Haiti na eneo zima.”Tukielekea Mashariki ya Kati huko Gaza, janga la kibinadamiu linaongezeka ambapo mashambulizi yanayoendelea yameathiri vibaya upatikanaji wa chakula na maji. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA, limeripoti kuwa usambazaji wa chakula kilichopikwa kaskazini mwa Gaza umepungua kwa asilimia 70, huku vituo vinne pekee ndivyo vinavyofanya kazi. Takriban watu milioni moja wanapata maji chini ya lita sita kwa siku, kiwango kilicho chini ya hali ya dharura.Nchini Sudan Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu Volker Türk ameonya kuhusu hali katika mji wa El Fasher, Darfur Kaskazin , akisema mji huo “uko kwenye ukingo wa janga kubwa zaidi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa kulegeza mzingiro wa kijeshi na kuwalinda raia,” huku Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) kikiongeza juhudi za kutwaa mji huo.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo ukumbi ni wake mlumbi wa Kiswahili Joramu Nkumbi kutoka nchini Tanzania, anafafanua maana za maneno "USHINZI NA USHENZI"Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!