
About
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania kupata ujumbe wa Zahra Salehe, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ICCAO linaloshughulika na masuala ya vijana amabye kwa kuwa mwaka huu 2026 ameshiriki tena katika mkutano wa CSW70 anatueleza ni kwa kiasi gani wameweza kulitekeleza malengo ya mikutano haya katika nchini humo.Vita Mashariki ya Kati vilivyoanzishwa na Marekani na Israeli dhidi ya Iran vikiingia mwezi wa pili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo hapa makao makuu ya UN jijini New York, Marekani amezungumza na waandishi wa habari akisisitiza sio tu vita hivyo vikome bali pia anaendeleza diplomasia za kusaka suluhu. Guterres amesema, Ninamtuma Mjumbe wangu Maalum Jean Arnault. Lengo ni kuunga mkono jitihada za kikanda. Lazima tupate njia ya amani ya kutoka katika hali hii. Ujumbe wangu uko wazi. Kwa Marekani na Israeli, ni wakati muafaka kusitisha vita vinavyosababisha mateso makubwa ya kibinadamu na tayari vinaanzisha athari mbaya za kiuchumi. Kwa Iran, isitishe kushambulia majirani zake.. Ripoti mpya ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kwa Uchumi wa Afrika, (ECA) imependekeza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi wa deni la umma barani Afrika, ikionya kwamba uendelevu hautegemei tu kiwango cha kukopa bali pia ubora wa taasisi, mifumo ya kisheria, na uwazi. Ikitolewa leo huko Addis Ababa, Ethiopia, ripoti hiyo inataja udhaifu kama vile uwezo mdogo wa kufanya uchambuzi wa hatari, na ushawishi wa mashinikizo ya kisiasa katika maamuzi ya kukopa ikisema kuwa kuboresha usimamizi ni jambo muhimu ili kuhakikisha kuwa deni la umma linachangia ukuaji wa uchumi endelevu badala ya kuwa chanzo cha kuyumba kifedha.Wakati dunia hii leo ikiadhimisha Siku ya Uelewa wa Usonji, familia katika Ukanda wa Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, zinakabiliwa na changamoto zinazoongezeka katika kuwahudumia watoto usonji katikati ya mzozo unaoendelea na hali mbaya ya kibinadamu. Katika kitongoji cha Sheikh Radwan kaskazini mwa Jiji la Gaza, Layan Abu Qousa mwenye umri wa miaka 16, ambaye ana usonji, anaishi na familia yake katika magofu ya nyumba yao. Familia yake inasema hali ngumu ya maisha imeongeza changamoto zinazohusiana na hali yake, huku ukosefu wa utulivu na mkwamo wa kupata huduma za kitaalamu ukiendelea kudhoofisha ustawi wake.Na katika jifunze Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye Kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “ATANGULIAYE KUFIKA HUCHAGUA PA KUKAA”Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!